Wednesday, 30 May 2018

Msichana na afya ya nywele

Wanasayansi wanakadiria kuwa, kichwa cha binadamu kina nywele kati ya 90,000 hadi 150,000 hivi, na kichwa ndiyo sehemu pekee ya mwili inayotazamiwa kuwa na nywele nyingi kuliko sehemu nyingine. Wasichana kama binadamu wengine wana nywele kila sehemu ya mwili isipokuwa katika viganja na nyayo za miguuni.
Wakati wa balehe nywele huongezeka makwapani na katika sehemu za siri. Ingawa siyo jambo la kawaida kwa wasichana kuota ndevu lakini inatokea wasichana wengine wanakuwa na ndevu, nywele kifuani, tumboni na hata mgongoni kwa wingi hali ambayo inafanya wawe na mtawanyiko wa nywele sawa na wanaume.
Nywele za mwilini ikiwa ni pamoja na nyusi, kope na nywele zinazoota sehemu zote zinafaida mwilini. Vinyweleo husaidia ngozi kuondosha takataka zilizo mwilini, pia husaidia ngozi isiathiriwe na vumbi pamoja na jasho. Nywele katika sehemu za siri pia husaidia kutunza ngozi ya sehemu hizo ambayo ni laini iwe safi na isipate muwasho pale inapotoa jasho jingi lenye chumvichumvi.
Nywele pia husaidia sehemu hizi za siri zisigusane na majimaji mengine yanayotoka mwilini hasa wakati wa tendo la ngono na kwasababu hiyo zinasaidia kupunguza uwezekano wa maambukizi ya magonjwa ya ngono kwa kiwango fulani.
Nyusi na kope husaidia jasho na vumbi visiingie ndani ya macho kwa urahisi. Kope pia hupunguza athari za mwanga wa jua kwenye macho. Kunyoa nyusi na kung’oa kope kunaweza kusababisha shida ya afya ya macho. Vumbi na jasho vinapoingia machoni husababisha muwasho wa macho na uvimbe wa ngozi laini ya macho, jambo ambalo hufanya macho yawe mekundu na kupata shida ya kuona vizuri hasa kwenye mwanga wa jua.
Kunyoa nyusi na kope pia kunaweza kutokeza michubuko ambayo huwapa nafasi bakteria kupenya ndani ya ngozi na kusababisha uambukizo wa ngozi ya macho na kusababisha magonjwa kama vile sekenene au chekea. Ni busara pia kuepuka kupaka rangi kwenye nyusi na kope kwani jambo hili linaweza kusababisha uambukizo, uvimbe au upofu wa macho kama rangi hizo zikiingia machoni kwa bahati mbaya.
Ili msichana awe na afya kamili ni lazima kuzingatia matunzo salama ya nywele. Ni vizuri kusafisha nyusi kila siku ili kuondoa vumbi na uchafu unaotokanan na kuganda kwa mafuta na vipodozi. Ni jambo linalopendeza kwa msichana kuchana nyusi kwa kitana na kuzipangilia vizuri ili zilete mwonekano unaovutia na urembo kwa msichana. Si vema kutumia cream zinazoondosha nyusi, hii inaweza kusababisha madhara kwenye macho kutokana na cream hizo zenye kemikali kuingia ndani ya macho au kusababisha muwasho kwenye ngozi.
Inashauriwa pia kuwa msichana asinyoe na kuondoa nywele zote na kuacha upara hasa katika sehemu zake za siri. Kufanya hivyo kunaweza kutokeza madhara ya kiafya hasa pale ngozi inapokuwa na michubuko midogomidogo inayotokana na makali ya wembe au kemikali ndani ya cream za kuondoa nywele. Michubuko hii inatoa mwanya kwa bakteria na virusi kupenya ndani ya mwili na kusababisha magonjwa.
Ngozi iliyoachwa wazi bila nywele pia hupata athari inapogusanan na jasho lenye takamwili. Ni vema nywele hizi zikapunguzwa kwa mkasi na kuwa fupi kadri inavyowezekana. Hii hufanya utunzaji wa sehemu za siri kuwa rahisi na kufanya ziwe safi bila madhara yoyote. Nywele zote zisafishwe kila siku kwa maji na sabuni na kukaushwa vizuri kwa kitambaa cha pamba au taulo safi.
Ile tabia ya kutokuoga kichwani kwa muda wa siku nyingi kutokana na kuvaa mawigi au kusuka, inaweza kusababisha athari za kiafya kwa mtumiaji. Uvaaji wa mawigi yaliyobana unaweza kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa mara. Lakini pia uvaaji wa mawigi unaweza kuharibu afya ya nywele za asili kutokana na ukweli kuwa nywele zinazofunikwa kwa muda mrefu ndani ya wigi, hukosa hewa na nywele hazipati mafuta ya asili ya mwili kulingana na mahitaji yake na hii inaweza kusababisha ngozi kukauka. Ngozi ya kichwa inapokuwa kavu, hupunguza uwezo wa nywele mpya kuota na kukua.
Pale inapobidi kuvaa wigi kutokana na sababu za msingi kama vile sababu za kitabibu, inashauriwa wigi lisivaliwe kwa zaidi ya saa sita kwa siku. Uvaaji wa wigi kwa saa 24 kila siku, unaambatana na athari za kiafya ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa vidonda katika ngozi ya kichwa na muwasho utokanao na magonjwa ya ngozi na mzio. Tatizo kubwa kutokana na uvaaji wa wigi, linaweza kusababishwa na kushindwa kuzisafisha nywele ipasavyo.
Nywele lazima zisafishwe mara kwa mara na kuzichana kwa chanuo au kitana kisichokata nywele kwa urahisi. Si vema kuchangia chanuo au kitana na watu wengine ili kuepuka kuambukizana magonjwa ya ngozi na chawa. Kama ni lazima na haiwezekani kuepuka hali hiyo basi kitana au chanuo lisafishwe vizuri kwa maji ya uvuguvugu na sabuni au spirit kabla ya kutumia kitana hicho.
Nywele zisizotakiwa katika sehemu yoyote ya mwili kama vile nywele zinazoota kuzunguka chuchu za matiti au kwenye kidevu zising’olewa bali zikatwe kwa mkasi ili kuepuka kusababisha uambukizo wa bakteria wanaopenya kwenye ngozi.
Mafanikio katika utunzaji wa nywele hutegemea kwa kiasi kikubwa afya ya mwenye nywele na nywele zenyewe. Afya ya nywele hutegemea vinasaba, lishe bora na mtindo bora wa maisha kwa ujumla. Nywele zenye afya nzuri ni zile zenye usawaziko sawia wa protini ngumu ya keratini pamoja melanin. Keratini huzipatia nywele nguvu na kuzifanya ziwe laini kwa ajili ya kutunzika vizuri.
Nywele zinaweza kupoteza afya yake pale zinapopungukiwa na Keratin, zinapochomwa kwa kipindi kirefu na mionzi ya jua (ultraviolet), joto kali, maji ya chumvi, magonjwa ya tezi la shingo pamoja na kemikali zilizomo ndani ya vipodozi au rangi za nywele. Upungufu wa madini ya zinc mwilini pia husababisha udhaifu wa nywele. Zinc husaidia tezi zenye mafuta zinazoshikilia nywele na vinyweleo ziwe na afya njema hivyo kuzifanya nywele na malaika zingine zisinyonyoke au kukatika kwa urahisi.

No comments:

Post a Comment

Toa Weusi Kwa (Pubic Areas) Mapajani na Kwapani Kwa Kutumia Hizi Simple Ingridients

Kuwa na Mapaja meusi au kwapa jeusi kweli ni issue wanayoface wanawake wengi sana so usishangae wala kwasababu ur not alone,mtu unakuwa na ...