Wednesday, 30 May 2018

Mavazi na afya

Mavazi yanaweza kuwa nguo, viatu, mikanda au miwani na kwa kawaida mavazi tunayovaa yana uhusiano wa karibu sana na afya pamoja na urembo wetu wa nje na moyoni. Ili kuelewa jambo hili ni vema kujiuliza kwa nini tunavaa mavazi? Ingawa zipo sababu nyingi zinazofanya watu tuvae nguo lakini kitabu cha kale zaidi cha historia ya mwanadamu kinaonyesha kuwa lengo la msingi kabisa la kuvaa nguo tangu mwanzo lilikuwa ni kumsitiri mtu na kuficha aibu ya uchi wa mwanadamu [14].
Leo nguo na mavazi mengine huvaliwa kwa ajili ya sababu nyingi ikiwa ni pamoja na kujilinda dhidi ya athari za hali ya hewa, mazingira, kazi na uchafu. Wengine huvaa nguo ili kuonyesha heshima katika jamii au kutokuwakwaza wengine. Wapo watu wengine wanaovaa mavazi kwa lengo la kujipamba na kupendeza.
Lakini kwa wengine mavazi huwa ni kitambulisho cha kazi kama vile nguo za michezo, sare za shule, nguo za askari, sare za wafungwa nk. Ingawa nguo zinaweza kumtambulisha mtu na kazi yake au tabia yake, watu wengine huvaa nguo ili kuficha utambulisho wao. Baadhi ya watu huvaa nguo kwa lengo la kuonesha uwezo wao wa kiuchumi katika jamii.
Ili kudumisha afya, msichana lazima avae nguo na mavazi mengine kutokana na sababu za kiafya –mwili, akili, roho, jamii, jinsia na afya ya mazingira. Inawapasa wasichana wanaojali afya zao kuvaa nguo zisizobana, zinazosetiri maungo vizuri na zenye kuheshimiwa katika jamii.
Mavazi yanayobana sana huzuia damu isitembee kwa uhuru katika mishipa yake. Jambo hilo husababisha ubongo kupata damu pungufu kuliko kawaida na kufanya ubongo usitende kazi yake sawasawa.Nguo zinazobana pia hufanya mwili usipate hewa ya oskijeni vizuri na kusababisha kutokwa jasho kwa wingi. Hii husababisha bakteria wanaokaa wenye ngozi wazaliane kwa wingi.
Msichana anayejiheshimu na mwenye adabu inampasa kuvaa mavazi yanayositiri mwili ambayo jamii inakubaliana nayo bila maswali. Huu ndio ushauri wa wazee walioheshimika katika zama zilizopita na wanazuoni wenye hekima [15]. ‘Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanaume, kwa maana kufanya mambo hayo ni kufanya machukizo’ hii ni kwa mujibu wa vitabu vya kale vya kumbukumbu za maadili na kanuni za afya ya jamii [16].
Hapa kinachozungumzwa siyo juu ya gauni, suruali au kanzu, jambo la msingi hapa ni kutambua ni mavazi ya aina gani katika jamii yako yanatambulika kama mavazi ya wanaume au wanawake. Kinachoshauriwa hapa ni kutokuvaa mavazi yanayoficha au kudhalilisha jinsia yako.
Vazi kama kitambulisho ni lazima likutambulishe kuwa wewe ni mtu wa jinsia gani. Likutambulishe kuwa wewe ni mwanamke au mwanaume na lilinde heshima ya jinsia yako. Hata hapo zamani watu walipokuwa wanavaa kanzu wanawake kwa wanaume, kulikuwa na alama au vigezo maalumu vilivyotambulisha vazi la kiume na lile la kike [17]. Katika jamii yetu leo pia yapo mavazi ambayo wasichana au wanawake wanayavaa na wanaume pia huyavaa bila tatizo lolote. Mfano mziri ni masweta, T-shirt au makoti.
Msichana ni lazima atambue mavazi yanayoshusha hadhi yake, aepuke mavazi ambayo mwenye hekima, mfalme Suleimani Daudi wa Israel ya kale aliyaita mavazi ya kikahaba [18]. Mavazi kama hayo yanaweza kuharibu afya ya kijamii ya msichana na kumwingiza katika hatari za kubakwa na ngono hatarishi.
Kwa kawaida mavazi ambayo si ya heshima yanasababisha watu wengi wasimfikirie msichana kwa mawazo safi. Jinsi tunavyovaa huongoza maoni ya wale tunao kutana nao katika maisha ya kila siku juu ya hali zetu za ndani na mtindo wa maisha tulio uchagua. Wavulana na wanaume wengi wenye tamaa ya ngono wanapomwona msichana aliyevaa mavazi ya kikahaba, wanatambua kuwa wanakaribishwa na msichana huyo kwa ajili ya kupata starehe ya ngono.
Mavazi pia yanaweza kuamua jinsi wengine wanavyotuwazia na wanavyotutendea, yanaweza kuonyesha sifa zilizomo ndani ya mtu na uwezo wake wa kufikiri na kutenda mambo, hasa wakati wa usaili kwa ajili ya ajira.
Mavazi mafupi sana yanayoacha mapaja wazi hayafai kwa msichana anayejiheshimu kwa sababu hayadumishi afya yake kijamii. Lakini pia mavazi marefu sana yanayoburuza chini aridhini nayo hayafai. Mavazi ya namna hii yanagusana na uchafu na yanakuwa kero zaidi wakati wa mvua au wakati wa kupita sehemu zenye matope na takataka zingine.
Viatu pia ni vazi la muhimu kwa msichana, vazi hili mbali na kutunza afya na kutuepusha ili tusipate maambukizi ya magonjwa, pia huongeza nakishi na urembo wa mvaaji. Kama mavazi mengine, viatu sharti vichaguliwe kwa lengo mahususi na kuzingatia afya kwanza kabla ya kutimiza malengo ya urembo na mvuto wa mvaaji.
Viatu vivaliwe kulingana na kazi, aina ya usafiri anaotumia au mahali anapokwenda mvaaji.Viatu vinaweza kuwa kwa ajili ya michezo, kazi maalumu, tukio maalumu au uvaaji wa kila siku kwa ajili ya afya.
Viatu vyenye kisingino kirefu sana mara nyingi si salama kwa afya kwani vinaweza kusababisha mteguko au maumivu ya miguu kwa urahisi.Viatu vya namna hii pia humchosha mvaaji haraka na kupunguza ufanisi hasa pale kazi yake inapohusisha kutembeatembea.
Viatu vya wazi ni vizuri zaidi kwa afya ya msichana hasa sehemu yenye joto jingi kwa vile husaidia miguu kupata hewa na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya ngozi yanayosababishwa na kuvu (fungus) na kupunguza uwezekano wa miguu kutoa harufu mbaya.
Miwani na mikanda pia inapovaliwa ni lazima izingatie matakwa ya kiafya. Kuna wasichana wengi leo wanaovaa miwani kwa lengo la kuongeza mvuto wao lakini wanafanya hivyo bila kupata au kuzingatia ushauri wa kitabibu kuhusu uvaaji wa miwani. Unaweza kukuta msichana anavaa miwani kwa sababu tu ameona wenzake wanaovaa miwani wanapendeza, hii hutokea mara nyingi kwa wanafunzi hasa katika shule za sekondali na vyuo vya elimu ya juu au miongoni mwa wasanii. Miwani imetengenezwa kwa makusudi na matumizi mbalimbali kama vile miwani ya jua au miwani ya ugonjwa wa macho hivyo vazi hili linapotumiwa ni vema likazingatia ushauri wa kitaalamu.
Mikanda au mishipi pia inapotumiwa kama vazi ni lazima ivaliwe kwa kuzingatia matakwa ya kiafya kwani kuvaa mikanda inayobana sana kunaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa kuzuia mzunguko huru wa damu mwilini.
Mikanda yenye vyuma vyenye madini ya Shaba pia inapovaliwa taadhari inahitajika sana kwani madini hayo na mengine yanaweza kusababisha ugonjwa wa ngozi pale mvaaji anapokuwa na tatizo la mzio (allergy) kwa madini hayo.

No comments:

Post a Comment

Toa Weusi Kwa (Pubic Areas) Mapajani na Kwapani Kwa Kutumia Hizi Simple Ingridients

Kuwa na Mapaja meusi au kwapa jeusi kweli ni issue wanayoface wanawake wengi sana so usishangae wala kwasababu ur not alone,mtu unakuwa na ...