Wednesday, 11 July 2018

Homa ya mitindo na fasheni katika ulimwengu wa sasa

Watu hawa kwa hakika wanafuata mitindo na fasheni ya aina fulani katika mavazi, katika kutengeneza na kukata nywele zao, katika harakati zao na kadhalika. Mitindo na fasheni (modality) ni jambo linaloonekana katika tamaduni na jamii zote, linapita katika jamii zote na kuwavutia watu mbalimbali.
Mwanadamu daima hukimbia hali ya kutobadilika (monotony), na kinyume chake anakaribisha mabadiliko, uvumbuzi na mageuzi. Mwanadamu ana hisi ya kupenda mabadiliko na uvumbuzi wa mambo mapya, na hisi hii nzuri hupendezesha dhahiri ya maisha yake. Kwa hakika hamu ya kupenda kujiremba, kuwa maridadi na kutengeneza vizuri mazingira ya maisha yetu ni jambo la kimaumbile linalotuhamasisha kuboresha mazingira tunamoishi. Hata hivyo inatupasa kuwa macho na makini mwenendo huo wa kupenda mabadiliko na mageuzi usije ikachupa mipaka na kuondoka katika hali yake ya kawaida, kwani viwapa vyote vya kimaumbile vinapotoka katika mkondo wake wa kimantiki huenda mrama na kumuingiza mwanadamu katika njia isiyo sahihi na ya upotofu na hatimaye kuwa na athari mbaya. Kwa mfano tu hamu ya kujipamba na kuwa maridadi ambayo inatokana na hisi ya kutafuta ukamilifu ya mwanadamu iwapo itaondoka katika mkondo wake wa kimaumbile itamtumbukiza mwanadamu katika mambo kama kujiona, kujigamba, kujiona mkamilifu, ubinafsi na homa ya fasheni na mitindo. Kila moja kati ya mambo hayo pia huwa sababu ya matatizo mengine kama kutumbukia katika hawaa na matamanio ya nafsi, mashindano ya kipuuzi, israfu na ufujaji na kadhalika na kuacha njia yake sahihi.  
Wimbi la fasheni na mitindo limegubika dunia ya leo
Hivi sasa katika zama za mawasiliano ambapo dunia imekuwa ndogo kama kijiji, mabadiliko yoyote yanayotokea katika mtindo wa maisha kwenye sehemu moja ya kijiji hiki huenea kwa kasi na kufika haraka sana katika sehemu nyingine za dunia. Mabadiliko na jipya lolote linalotokea katika mambo mbalimbali kama mitindo ya mavazi, jinsi ya kujiremba, mazingira, fasheni na modeli za magari, fasheni za mikoba, vyombo vya nyumbani na hata misamiati ya kisiasa, jinsi ya kuamkuana na kadhalika huenea haraka katika maeneo mengine na bila ya kujua, tunawaona vijana katika jamii mbili tofauti wakiwa na mienendo inayoshabihiana ambayo kwa hakika inatokana na kufuata mtindo na fasheni moja.
Katika mtazamo wa awali huwenda hali hii ikawa jambo la kuvutia, kwa sababu hisi ya kupenda umaridadi na uzuri imewekwa katika dhati ya mwanadamu, na dini tukufu ya Uislamu haipingi suala hilo la kimaumbile. Si hayo tu bali dini hiyo imewataka wafuasi wake kuwa maridadi, wasafi, wenye sura na dhahiri nzuri na kuwa mbali na maisha ya aina moja na yasiyo na harakati ya mabadiliko ya kuelekea kwenye ukamilifu. Hata hivyo kengele ya hatari husika pale kufuata fasheni na mitindo kunapogeuka na kuwa homa au kitu kinachoshabiana na ibada ya fasheni na mitindo, na wakati huu huwa vigumu sana kwa vijana wengi kujua thamani zao za kiitikadi na kiutamaduni, kupambanua baina ya sahihi na lisilo sahihi na hatimaye hujikuta wametumbukia katika mienendo inayokinzana na thamani, utamaduni na maadili ya jamii zao. Suala hili linaonekana zaidi katika nchi zinazostawi za ulimwengu wa tatu na limewatia wasiwasi mkubwa wataalamu wa masuala ya jamii na mienendo ya binadamu.
Dokta Ghulamali Afrooz ambaye ni mtaalamu wa saikolojia na mhadhiri wa vyuo vikuu nchini Iran anaamini kuwa, mabarobaro na vijana wengi waliotumbukia katika janga la uraibu wa fasheni na mitindo na wanaovaa mavazi yasiyo ya kawaida, kwa hakika wanasumbuliwa na mashaka na maumivu ya kinafsi na kiroho. Mtaalamu huyo maarufu wa masuala ya kisaikolojia anasema: Aghlabu ya watu wa aina hiyo hawakupata mapenzi ya kutosha ya baba na mama zao, na haki zao za kiroho hazikuchungwa ndani ya familia. Kwa msingi huo moja ya sababu za matatizo hayo ya uraibu wa fasheni na mitindo ni nakisi na matatizo ya kinafsi. Kupuuzwa na familia hususan wazazi wawili, kutopongezwa na kushajiishwa na ukandamizaji wa mara kwa mara wa mtoto ni miongoni mwa mambo yanayomsukuma katika tabia za kutaka kujiona na kujionesha mbele za wengine. Inasikitisha kuwa, katika kipindi cha sasa hususan katika miongo kadhaa ya hivi karibuni, fasheni na mitindo vimefikia kiwango cha uraibu na kuchupa mipaka na baadhi ya vijana wanafanya jitihada za kutaka kujionesha na kudhihirisha uwepo wao kwenye jamii kwa kuvaa suruali zilizochanika kwenye magoti au mapaja, nguo za nusu uchu, kujichora tatoo kwenye viungo mbalimbali vya mwili, kutoboa viungo hivyo kama midomo chini ya nyusi za macho na kadhalika", mwisho wa kunukuu.
Kwa upande wake, Dokta Hassan Balkhari ambaye ni mtaalamu wa umagharibi (Westology) na mhadhiri mashuhuri wa vyuo vikuu nchini Iran amechambua suala la fasheni na mitindo katika upande wa masuala ya kijamii na kisiasa na kutoa mtazamo wa kutiliwa maanani kuhusu mikono ya nyuma ya pazia ya fasheni na mitindo hiyo. Anasema: Baada ya kusambaa fikra ya utandawazi hususan katika masuala ya kiuchumi, dunia iligawanywa katika kambi mbili, kambi ya kaskazini kwa maana ya kambi yenye utajiri na nguvu, na kambi ya kusini ya nchi maskini na dhaifu. Kwa utaratibu huo- anaendelea kusema Dokta Hassan Balkhari- tumeingia katika anga mpya ambayo kigezo chake ni utajiri na nguvu. Wakati kigezo cha kuigawa dunia kinapokuwa utajiri na nguvu za kimaada, baadhi ya watu wanaotaka kudhibiti dunia hufanya jitihada za kuwa na taathira katika fikra na maoni ya waliowengi. Udhibiti huu una sura na pande mbalimbali na moja kati ya sura zake ni kuanzisha fasheni na mitindo ya aina mbalimbali. Kambi ya utajiri na nguvu hufanya jitihada za kuwasukuma watu wote katika anga mpya isiyokuwa na vigezo vya hapo kabla. Matokeo yake ni kwamba, fasheni na mitindo mipya hujaza anga ya maisha ya mwanadamu na kuyafanya maisha yake kuwa anga ya mtumiaji tu na mfuasi wa mitindo na fasheni za mwenye nguvu na utajiri. Katika anga hiyo mpya, mwanadamu hupotea njia ya kutafuta ukamilifu wake halisi", mwisho wa kunukuu.
Kwa maelezo hayo ya wataalamu wa masuala ya umagharibi na elimu nafsi, tunaelewa kuwa, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na zana za mawasiliano ya umma za Magharibi havina nia ya kutaka kujaza wakati wa mapumziko na faragha wa vijana bali kanali za televisheni za satalaiti, filamu za Hollywood, michezo ya kuigiza na kadhalika yote yana malengo na majukumu maalumu. Makampuni mengi ya kibiashara na ya uzalishaji pia yamekuwa yakitumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kudhamini utengenezaji wa filamu mbalimbali na kutangaza fasheni na mitindo yao kupitia mavazi, muonekano na mienendo ya nyota wa filamu hizo na kwa njia hiyo kuwavutia watazamaji katika bidhaa na tamaduni zao.
Kufuata mitindo na fasheni kibubusa na bila ya kujali mipaka ya itikadi, utamaduni na maadili kuna gharama kubwa kwa wafuasi wa fasheni hizo na jamii zao, na faida kubwa kwa makampuni yanayotengeneza na kubuni fasheni na mitindo hiyo na vilevile kwa tawala au mifumo inayotaka kutandawazisha fikra na kile wanachokiita "thamani na maadili ya Kimagharibi (values)". Makampuni hayo pia yanawekeza sana katika mashindano ya michezo ya kitaifa na kimataifa na kuwadhamini watu mashuhuri na wanamichezo bingwa kwa ajili ya kutangaza bidhaa za makampuni hayo na kueneza maadili na tamaduni za Kimagharibi. Makampuni hayo hufanya jitihada za kutangaza mavazi ya nyota hao, aina ya mishono ya mavazi yao, rangi za mavazi yenyewe, mitindo yake makhsusi, jinsi ya kutengeneza na kuremba nywele na sura zao, bangili na mikufu yao na kuzifanya kuwa alama ya kibiashara na fasheni ya kisasa. Kwa msingi huo kutumia fasheni na mitindo hiyo kunaweza kuwa na maana ya kushikamana na kundi, fikra na utamaduni fulani, kuukubali, kuupenda, kuwa na itikadi na fikra zake na za watu wanaovaa mitindo hiyo, kuwatangaza na kuonesha mshikamano na wao.
Homa ya kufuata mitindo na fasheni mbali na hasara zake za kifedha na kupoteza utambulisho wa mtu, wakati mwingine huwa na madhara kwa mwili na afya ya mtu. Madaktari wanasema, zana na bidhaa nyingi zinazotengenezwa na makampuni ya mitindo na fasheni hazizingatii afya na siha ya watumiaji wake. Hii ni baada ya kuthibitika kwamba, maradhi mengi ya mwili kama maumivu ya miguu, mgongo, aina mbalimbali za saratani, matatizo ya homoni na neva na kadhalika yanatokana na utumiaji wa bidhaa zisizo na viwango vya afya za makampuni hayo yanayotanguliza mbele muonekano wa mtu, mvuto na dhahiri yake. Nguo za kubana maungo ya mwili, vipodozo visivyozingatia viwango vya usalama wa mwili na afya, vyuma visivyo salama kwa afya ya mwanadamu vinavyotumiwa kwa ajili ya tundu za midomo, pua na maungo mengine ya mwili, vyote vina madhara makubwa ya kiafya kwa mwili wa mwanadamu.    

No comments:

Post a Comment

Toa Weusi Kwa (Pubic Areas) Mapajani na Kwapani Kwa Kutumia Hizi Simple Ingridients

Kuwa na Mapaja meusi au kwapa jeusi kweli ni issue wanayoface wanawake wengi sana so usishangae wala kwasababu ur not alone,mtu unakuwa na ...