Maziwa hufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya afya yako. Wataalamu wa afya na wauzaji wa maziwa wamekuwa wakieleza faida kadha wa kadha za kunywa maziwa. Je umewahi kujiuliza hasa ni faida gani hizo zitokanazo na unywaji wa maziwa?
Ni wakati wako sasa wa kujiuliza kwa kina juu ya faida zitokanazo na unywaji wa maziwa. Fuatana nami katika makala hii nikueleze faida 10 zitokanazo na unywaji wa maziwa.
1. Hujenga na kulainisha ngozi
Je unamfahamu Cleopatra? Cleopatra alikuwa ni malikia wa Misri anaesadikiwa kuwa mzuri sana. Inaaminikia uzuri wa Cleopatra ulitokana na tabia yake ya kuogea maziwa mara kwa mara.
Hivyo basi, ni wazi kuwa, vitamini na virutubisho vilivyoko katika maziwa ni muhimu kwa ajili ya ngozi bora. Ni vyema kunywa angalau bilauri moja ya maziwa kila siku.
2. Huimarisha meno
Maziwa ni chanzo bora cha madini ya kalisiamu, hivyo basi maziwa ndicho kitu halisi kinachohitajiwa na meno yetu. Pia maziwa huzuia kutoboka na kuoza kwa meno. Kalisiamu hufyonzwa na miili yetu kukiwa na vitamini D; hivyo jitahidi kunywa maziwa kwani maziwa huwa na vitamini D.
3. Huimarisha mifupa
Ni ukweli usiopingika kuwa watoto wanahitaji kunywa maziwa ili kuimarisha ukuaji wao. Ni kweli pia watu wazima wanahitaji kunywa maziwa ili kulinda na kuimarisha mifupa yao dhidi ya magonjwa kama vile udhaifu wa mifupa (osteoporosis). Maradhi haya huzuiliwa kwa kalisiamu ipatikanayo kwenye maziwa na ambayo hufyonzwa kutokana na uwepo wa vitamini D.
4. Kujenga misuli
Maziwa yana mchango mkubwa katika ukuaji wa misuli. Hili ni kutokana na protini zinazopatikana katika maziwa. Wanariadha wengi hunywa maziwa baada ya mazoezi, hii ni kwa ajili ya kuupa mwili virutubisho vya kutosha kwa ajili ya kujijenga tena. Maziwa huzuia maumivu ya misuli pamoja na kurudisha ute ulipotea kwenye misuli wakati wa kazi mbalimbali.
5. Kupunguza uzito
Utafiti unaonesha kuwa wanawake wanaokunywa maziwa hupunguza uzito zaidi kuliko wale wasiokunywa. Inashuriwa kunywa maziwa wakati wa chakula cha jioni au unapokula matunda. Pia maziwa yanaweza kutumiwa kama kileta hamu ya kula yaani appetizer.
6. Huondoa msongo wa mawazo
Hebu fikiri juu ya vitamini na virutubisho vilivyoko kwenye maziwa; hivi huweza kuondoa msongo. Baada ya kazi nyingi za siku, inashauriwa kunywa angalau bilauri (glass) moja ya maziwa ya uvuguvugu. Hili litakusaidia kukuondolea msongo katika misuli na neva zako za fahamu.
7. Huzuia maumivu wakati wa hedhi
Wanawake wengi wanakabiliwa na maumivu wakati wa hedhi. Maziwa yamedhibitishwa kuzuia na kupunguza maumivu haya kwa kiasi kikubwa.
8. Huongeza nguvu za mwili
Je unaishiwa nguvu mapema au kuchoka sana? Kama jibu ni ndiyo, unahitaji virutubisho vilivyoko kwenye maziwa. Hivi vitaupa mwili wako nguvu mpya na kukufanya kuwa mwenye nguvu na furaha siku nzima.
9. Huondoa kiungulia
Kiungulia huwasumbua sana watu wengi. Kiungulia husababishwa na asidi zipatikanazo tumboni. Hivyo maziwa (ambayo si mgando) hutengeneza utando maalumu tumboni ambao hupambana na asidi hizi.
Kwa hiyo nywaji wa maziwa (ambayo si mgando) utakusaidia kupambana na tatizo la kiungulia ndani ya muda mfupi.
10. Hupambana na maradhi mengine
Kwa miongo kadhaa tafiti zimebaini kuwa maziwa huzuia magongwa kadha wa kadha. Magonjwa hayo ni kama vile shinikizo la damu na kiharusi. Inaaminika pia maziwa hupunguza lehemu (cholesterol) mwilini na kuongeza uwezo wa macho kuona. Baadhi ya watafiti wameeleza kuwa unywaji wa maziwa huzuia ania fulani za saratani.
Hitimisho
Yaliyozungumziwa hapa ni faida 10 za kunywa maziwa. Naamini umebaini kuwa maziwa yana manufaa mengi sana kwa ajili ya afya yako zaidi ya haya yaliyotajwa. Ni jambo jema kujizoesha kula vitu vya asili, kwani ndivyo huhitajiwa zaidi na mwili wa mwanadamu. Jizoeze kunywa angalau bilauri moja ya maziwa kila siku kwa ajili ya afya ya mwili wako.
Je una maoni gani kuhusu makala hii? Je wewe huwa unakunywa maziwa? Tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe na wengine. Karibu pia ufuatilie ukurasa wetu wa Facebook ili ufahamu mengi zaidi.
No comments:
Post a Comment